Jumamosi, 29 Agosti 2015

Msenegal mwingine kitanzini Simba


Pape Abdoulaye N'daw
Hatma ya Msengal wa pili katika wiki moja ndani ya Simba itaanza kujulikana leo wakati Pape Abdoulaye N’daw leo atakapopewa mtihani wa kwanza na kocha Dylan Kerr, Zanzibar.
 
Simba iliachana na mipango ya kumchukua Papa Niang baada ya dakika 45 za mechi ya kirafiki katikati ya wiki, ilipogundua kuwa ni 'bomu'.
N'daw naye atakuwa na mtihani rasmi wa kwanza Simba wakati mabingwa wa Bara wa zamani hao watakapocheza kirafiki dhidi ya Mafunzo kwenye uwanja Uwanja wa Amaan.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema N’daw aliyetokea klabu ya Dinamo Bucuresti ya Ligi Kuu ya Romania atacheza pia mechi nyingine Jumapili dhidi ya JKU.
 
“Baada ya mechi hizo mbili, naamini benchi la ufundi litakuwa limeona uwezo wake na kuamua kama asajiliwe au aachwe aende," alisema Hans Poppe na kuahidi "tutasubiri kauli ya kocha wetu juu ya uwezo wake.”
Aidha, Hans Pope alisema mchezaji kutoka Mali, Makan Dembele ataungana na Simba Zanzibar pindi atakapofika.
 
 “Kumekuwa na vikwazo katika safari yake, lakini tunadhani leo (jana) atafika na akifika tutampeleka Zanzibar kuungana na wachezaji wengine ambapo pia Kocha Kerr atatoa maamuzi yake baada ya kumuangalia uwanjani.
 
Benchi la ufundi la timu hiyo liliachana na Niang baada ya kumjaribu kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Mwadui kwenye Uwanja wa Taifa Jumatatu.  
 
Kocha wa Simba, Kerr amewaagiza viongozi kumtafutia mshambuliaji mwenye uwezo juu baada ya kuona waliopo wanashindwa kuzitumia vizuri nafasi za kufunga zinazopatikana.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni