Katika mikutano yote mikubwa kwa midogo aliyoianza wiki hii,
alisimama na kumwaga ahadi kwa wananchi lakini jana alisimama mara moja
katika mikutano miwili na kushindwa kuongea baada ya sauti kukwama.
Licha ya kujitahidi kuzungumza, sauti ilikwama na kumlazimu
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, kuwanadi wagombea wa
majimbo ya Rugwe na Busokelo na Dk. Magufuli kumalizia kwa kuomba kura.
Akiwa njiani kwenda Kyela, alisimama Kiwira kuwasalimu wananchi
waliofunga barabara, lakini alipojaribu kusema “CCM hoyee…” sauti
haikutoka licha ya kurudia na baadaye kutoka kwa kukwaruza.
Katika eneo hilo alisema ameomba nafasi ya urais ili aweze kuleta
maendeleo ambayo hayana chama na kwamba yataonekana mara moja mwakani,
kama kutoa elimu bure na hiyo itawezekana kwa kuwa mafisadi watakuwa
wamedhibitiwa.
Akihutubia wananchi wa Kyela katika uwanja wa John Mwakangale,
baada ya sauti kugoma, aliwaeleza wananchi hao kuwa "bahati mbaya sauti
yangu siyo nzuri, najua Mungu wangu atairudisha kwa jina la Yesu,"
alisema na alipojaribu kusema “Kyela hoyee…” sauti haikutoka.
"Nilitamani nimwage sera za kutosha lakini sauti yangu siyo nzuri,
nashindwa kuongea, wapinzani wameniloga washindwe na walegee kwa Jina la
Yesu.mnaona jina la Yesu limeanza kufanya kazi," alisema.
Hali hiyo iliendelea wakati akihutubia Rugwe na kumlazimu
Mwenyekiti wa mkoa kuwanadi wagombea ubunge na Mjumbe wa Halmashauri Kuu
(Nec) William Lukuvi, kutoa ahadi kwa niaba ya mgombea na kumkaribisha
ambaye hakuongea muda mrefu.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Zambi akihutubia wana Kyela
alisema chama hicho hakikubahatisha kumpata mgombea urais na kwamba
waliodhani wamepotea ukweli ni kwamba chama kiko imara kuliko awali.
Dk. Magufuli akizungumza na wananchi hao alisema ameomba nafasi ya
urais kwa kuwa anaweza na kuomba vyama vyote kumchagua bila kujali
itikadi zao kwa kuwa maendeleo hayana chama na kwamba changamoto za
Watanzania anazifahamu na yupo tayari kuzitatua.
Aidha, aliahidi kutengeneza kwa kiwango cha lami barabara ya Matema
Beach hadi Kyela itakayogharimu Sh. bilioni 56 na kwamba mkandarasi
yupo kazini kuhakikisha ujenzi unaanza.
Alisema akiwa rais atahakikisha waendesha pikipiki hawasumbuliwi na
askari wa usalama barabarani, na mama lishe kutozwa kodi ambazo ni
usumbufu na kwamba watatoa mikopo kwa kila kata.
Alisema atajenga barabara ya kilometa 80 kwa kiwango cha lami, na
kwamba alipokuwa Waziri wa Ujenzi alikuwa anaagizwa ila kwa sasa
ataagiza na kazi zitafanyika.
Kadhalika aliahidi maji safi na salama kwa wanachi na kuongeza:
"Wapo wanaosema CCM imechoka, jamani nauliza mimi nimechoka? Ili uwe
rais unatakiwa uwe kiongozi wa watu, nimeomba kufanya kazi na siyo
kufanyiwa kazi nitumeni kazi sasa,"alisema.
Aliahidi kuteua mawaziri watakaofanya kazi usiku na mchana na kwa
kasi atakayokuwa nayo wapo watakaokimbia na kuwaomba wananchi hao
kumchagulia wabunge na madiwani wa kutosha ili aunde serikali.
Lukuvi akiongea na wananchi hao, alisema Tanzania jembe ni moja
ambalo ni Dk. Magufuli na lipo tayari kwa kazi za kuwatumikia wananchi.
Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, alisema Dk.
Magufuli ni mwadilifu, mnyenyekevu, makini, mzalendo na si fisadi na
kwamba anastahili kuvikwa joho la urais.
Alisema urais ni taasisi anayokabidhiwa mcha Mungu, anayekuwa
jemedari wa majeshi yote hivyo akiwa hana upendo au fisadi anaweza
kushauriwa na mkewe kuiingiza nchi matatizoni.
CHANZO:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni