UMUHIMU WA KUWEKA IMANI YAKO KATIKA
JINA LA YESU KRISTO
“Basi Petro na Yohana
walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali , saa tisa. Na mtu
mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye
walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa
watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia
hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana,
akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro
akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho.
KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI, simama uende. Akamshika mkono wa kuume,
akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka
upesi akasimama, akaanza kwenda …” (Matendo ya Mitume 3:1 – 8)
Ukifuatilia
historia ya kilema huyu aliyeponywa utaona ya kuwa alikuwa hivyo tangu
kuzaliwa, na alipopona alikuwa na umri uliopita miaka arobaini (Matendo ya
Mitume 4:22).
Siri
ya muujiza huu ilikuwa ni nini? Je! kilema huyu alipona kwa uweza wa Petro na
Yohana au kwa uweza wa jina la Yesu Kristo?
Nauliza
maswali haya kwa kuwa watu wengi wakimwona mtu anatumiwa na Mungu katika
uponyaji wanaweka imani katika mtu huyo badala ya kuweka imani katika jina la
Yesu Kristo.
Na ndivyo ilivyokuwa wakati kilema huyu
alipopona, watu waliokuwa hekaluni waliwashangaa wakina Petro na Yohana kama
vile kilema huyo alipona kwa uwezo wao. Petro alipoona hali hiyo, aliamua
kuwaeleza watu hao ukweli ulivyo; alisema hivi;
“Basi (Yule aliyekuwa kilema) alipokuwa
akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile
lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya
akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia
macho sisi, kama kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi au kwa utauwa
(utakatifu) wetu sisi?” (Matendo ya Mitume 3:11 – 12).
Petro alikuwa
anafanya jambo muhimu hapa kwa kusaidia kubadilisha mawazo ya watu ya kufikiria
kuwa uwezo uliomponya kilema ulikuwa ni wa Petro na Yohana ambayo haikuwa si
kweli. Kama uwezo huu haukuwa wao, muujiza huu siri yake ni nini? Petro
aliendelea kusema hivi;
“Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo,
Mungu wa Baba zetu, amemtukuza mtumishi
wake Yesu ….. Na kwa IMANI KATIKA JINA LAKE, JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile
iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele zenu ninyi nyote” (Matendo ya Mitume
3:13 – 16).
Hebu
tafakari maneno haya ya Petro; “Na kwa IMANI KATIKA
JINA LAKE JINA LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU….” Wakina Petro na Yohana
waliweka imani yao katika jina la Yesu Kristo. Walikuwa na uhakika mioyoni mwao
kuwa siri ya miujiza imo katika jina la Yesu Kristo – ndiyo maana walipomkuta huyo kilema walimwamuru asimame
kwa jina hilo!
Weka
imani yako katika jina la Yesu Kristo ukitaka kuona ishara na miujiza ya Yesu
Kristo maishani mwako na kwa wale unaowahudumia pia. Wakijua hili wanafunzi wa
kwanza wa Yesu Kristo walipokatazwa “wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina
la Yesu” na Anasi kuhani mkuu, waliomba wakasema; “…Basi
sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako
kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ISHARA NA MAAJABU vifanyike kwa
JINA LA MTUMISHI WAKO MTAKATIFU YESU” (Matendo ya Mitume 4:18,29 –
31)
Ni muhimu kuwaeleza na kuwakumbusha watu umuhimu wa kuweka imani zao katika jina la Yesu Kristo wakitaka kuona mkono wa Bwana ukiponya, ukifanya ishara na miujiza.
Ni muhimu kuwaeleza na kuwakumbusha watu umuhimu wa kuweka imani zao katika jina la Yesu Kristo wakitaka kuona mkono wa Bwana ukiponya, ukifanya ishara na miujiza.
Nakumbuka
kuna mama mmoja alifika nyumbani kwangu akiwa anaumwa sana toka mkoa mwingine
nje ya mkoa huu wa Arusha ninaokaa.
Baada
ya mahojiano naye nilifahamu ya kuwa ameugua bila kupona kwa muda wa miaka
miwili. Na katika miaka hiyo miwili amezunguka kwa watu mbalimbali kuombewa
bila mafanikio. Alipoona haponi akaenda kwa waganga wa kienyeji ambako nako
hakupona. Alipoona kwa waganga wa kienyeji haponi akaanza kutafuta watu
wamuombee tena.
Katika
mazungumzo hayo nilitambua kuwa anapokwenda kuombewa anaweka imani yake katika
watu wanaomuombea na wala haweki imani yake katika jina la Yesu Kristo.
Nilifungua
Biblia yangu na nikaanza kuzungumza naye juu ya uweza wa jina la Yesu Kristo,
na umuhimu wa yeye kuweka imani yake katika jina la Yesu Kristo na siyo kwangu.
Mwishoni nikamuuliza kama ameelewa na ikiwa yuko tayari kwa maombi kwa
kulitumia jina la Yesu Kristo.
Yule
mama akajibu akasema; “Ndiyo nipo tayari kwa kuombewa, naamini kwa jina la Yesu
Kristo nitapokea uponyaji”
Mara
nilipoanza kuomba, aliangushwa chini na mapepo yaliyojidhihirisha toka ndani
mwake. Nikayaamuru mapepo hayo yamtoke mama yule kwa JINA LA YESU KRISTO – na
mara hiyo yakamtoka na akawa mzima!
Ugonjwa
uliomsumbua kwa muda wa miaka miwili ulitoweka, yule mama pamoja na mume wake
aliyemsindikiza waliondoka kwa furaha huku wakimsifu Mungu kwa matendo makuu
aliyowatendea.
Kumbuka Petro
alisema; “… Kwa IMANI katika JINA LAKE (YESU) , JINA
LAKE LIMEMTIA NGUVU MTU HUYU ….”
Atakayeliitia jina la
Bwana ataponywa :
Nabii
Yoeli alitabiri kuwa; “Na itakuwa ya kwamba mtu
awaye yote ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAPONYWA; kwa kuwa …. Watakuwako watu
watakaookoka, kama Bwana alivyosema;” (Yoeli
2:32).
Mtume Paulo alitilia mkazo utabiri huu aliposema;
“Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na
Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;
kwa kuwa, KILA ATAKAYELIITIA JINA LA BWANA ATAOKOKA (Warumi 10:12 –
13).
Kila anayeliitia jina la Bwana Yesu kwa imani anaponywa na, anaokoka kwa kuwa
ndani ya jina hili la Yesu Kristo mna uponyaji na wokovu kwa kila amwaminiye
Yesu Kristo.
Lakini
Mtume Paulo anauliza swali muhimu ambalo ni vizuri kulitafakari; anasema; “Basi wamwitaje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye
wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? (Warumi 10:14).
Hili
jambo ni kweli. Huwezi kumwita mtu usiyemwamini. Hii ina maana ya kuwa ikiwa
tunataka watu waliitie jina la Yesu ili waokoke na kuponywa madhaifu yao,
inatubidi tuhubiri na kufundisha juu ya Yesu na jina lake.
Ndiyo
maana Bwana Yesu Kristo alimwambia Anania ya kuwa Paulo “ni chombo kiteule kwangu, ALICHUKUE JINA LANGU, mbele ya
Mataifa, na Wafalme, na wana wa Israeli” (Matendo ya Mitume 9:15).
Biblia
inasema pia kuwa; “Filipo akatelemka akaingia mji
wa Samaria, AKAWAHUBIRI KRISTO. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno
yale yaliyosewa na Filipo, walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya
kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu;
na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule” (Matendo ya Mitume
8:5 – 8).
Smithi
Wigglesworth aliyekuwa mhubiri wa huko Uingereza katika miaka ya 1930 aliwahi
kushuhudia katika mahubiri yake kuwa siku moja aliitwa kwenda kumuombea mgonjwa
mmoja wa kifafa aliyekuwa amezidiwa hata kushindwa kuamka.
Anasema
watu wa eneo lile na hata ndugu zake yule mgonjwa walikuwa wamekata tamaa.
Waliona ndugu yao atakufa kwa ugonjwa huo. Kwa hiyo ilimchukua muda Bwana Smith
Wigglesworth kupata walio tayari kushirikiana naye katika kumuombea mgonjwa
yule.
Mwishoni
alifanikiwa kuwapata, na anasema walikizunguka kitanda cha yule mgonjwa na
wakaanza kuliitia jina la Yesu kwa pamoja wakisema “Yesu, Yesu, Yesu, Yesu,….”
Kwa kulirudiaruda jina hili. Baada ya kuliitia jina la Yesu kwa muda hivi,
anasema nguvu za Mungu zilishuka kitandani kwa yule mgonjwa, zikamtingisha
mgonjwa na kitanda chake.
Yule mgonjwa akapona saa ile ile, akavaa nguo na kutoka nje. Kijiji kizima
kilitaharuki na kushangaa kilipomuona mtu yule amepona. Smith Wigglesworth
alipoona watu wamekusanyika hivyo wakishangaa, alichukua Biblia yake akahubiri,
na watu wengi walikata shauri na kuokoka siku ile.
Ni
muhimu ufahamu ya kuwa muujiza unaofanywa kwa jina la Yesu Kristo unawavuta
watu kwa Yesu Kristo, wamwamini na kumfuata.
Ndiyo maana imeandikwa juu ya Yesu Kristo kuwa;
“Hata (Yesu Kristo) alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi WALIIAMINI JINA LAKE, walipoziona ishara zake alizozifanya” (Yohana 2; 23).
“Hata (Yesu Kristo) alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi WALIIAMINI JINA LAKE, walipoziona ishara zake alizozifanya” (Yohana 2; 23).
Siku
moja nilikuwa katika sehemu fulani nikifundisha juu ya jina la Yesu Kristo.
Mwisho wa somo nilisema watu wanaotaka kujazwa na Roho Mtakatifu na wanene kwa
lugha mpya pamoja na wagonjwa waje mbele. Watu wengi walikuja mbele.
Niliwaambia
hatutaomba neno lolote zaidi ya kuliitia jina la Yesu kwa pamoja na kwa
kulirudiarudia. Kwa pamoja tukaanza kuliitia jina la Yesu tukisema kwa sauti;
“Yesu, Yesu, Yesu, Yesu…..”
Muda
haukupita mwingi, tukiwa bado tunaliitia jina hili nikasikia toka upande wangu
wa kushoto sauti ya maji mengi yakiporomoka. Nilijua hii ni ishara ya uwepo wa
Roho Mtakatifu kwani mahali tulipokuwapo hapakuwa na mto wowote karibu, wala
mvua ilikuwa hainyeshi. Baadaye nilipowaeleza watu juu ya sauti hiyo ya maji,
kuna wengine pia waliosema kuwa waliisikia.
Tulipoendelea
kuliitia jina la Yesu Kristo, wagonjwa walipona, waliokuwa na mapepo walipona,
na wengine walijazwa Roho Mtakatifu na wakazungumza kwa lugha mpya. Ishara na
miujiza mingi ilifanyika kwa kuliitia jina la Yesu Kristo.
Kumbuka
Yesu Kristo alisemal “Na ishara hizi zitafuatana na
hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya…”
(Marko 16:17 –18).
Hukumu kwa kutoliamini jina la Yesu :
“Amwaminiye
yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu HAKULIAMINI jina
la Mwana pekee wa Mungu” (Yohana 3:18).
Usipoliamini
jina la Mwana pekee wa Mungu – jina la Yesu Kristo ujue umekwisha kuhukumiwa.
Hii ina maana ya kuwa unapoteza wokovu; - unapoteza ushindi; - unapoteza uzima
wa milele; - na pia bado unakaa katika mauti! Hebu soma na kutafakari mistari
ifuatayo ili uone umuhimu wa kuliamini jina la Yesu Kristo:
“Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na
lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda
yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba TULIAMINI JINA LA
MWANA WAKE YESU KRISTO, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri” (1Yohana
3:21 – 23).
“Bali wote waliompokea (Yesu Kristo) aliwapa uwezo wa kufanyika
watoto wa Mungu, ndio wale WALIAMINIO JINA LAKE” (Yohana
1:12).
“Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na
huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu; hiyo imani yetu. Mwenye kuushinda
ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?
…. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu
umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa
Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa, mna
uzima wa milele, ninyi MNAOLIAMINI JINA LA MWANA WA MUNGU” (1Yohana 5:4-5; 11 – 13).
“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana
JINA jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa
kwalo” (Matendo ya Mitume 4:12) – isipokuwa ni JINA LA YESU KRISTO!
MUHIMU :
Kama
tulivyokwisha kukuandikia katika sura ya tatu ya somo hili – ukitaka kulitumia
jina la Yesu Kristo kihalali na uweze kuona uwezo na mamlaka yake ni muhimu:
Kwanza: Uwe mwana wa Mungu kwa kumpokea Yesu Kristo moyoni mwako kama
Bwana na Mwokozi wako;
Pili: Uwe mtii ukifuata maagizo ya neno la Kristo katika Roho
Mtakatikfu.
Kuna
watu wengine wanataka kuwa watii kufuata maagizo ya neno la Kristo huku
hawapendi kuokoka. Hawajui utii bila kuokoka ni utii nusu – ukitaka uone
muujiza wa jina la Yesu Kristo katika maisha yako inabidi ufanye yote mawili –
uokoke na utii.
Ikiwa
hujaokoka na unataka uokoke sasa isome sala ifuatayo kwa sauti (ikiwezekena
upige magoti) mahali pa utulivu huku ukiamini ya kuwa Mungu anakusikia:
“Ee Mungu wangu Mtakatifu.
Nimesikia neno lako nami nimeamini. Naomba unisamehe dhambi zangu zote
nilizokukosea katika maisha yangu yote. Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa
ajili yangu, naomba initakase sasa katika roho yangu, nafsi yangu na mwili
wangu. Nimefungua moyo wangu sasa; Ee Bwana Yesu Kristo nakuomba uingie ndani
yangu, uwe Bwana na Mwokozi wangu kuanzia sasa na siku zote. Ahsante kwa
kunisamehe dhambi zangu na Ahsante kwa kuniokoa. Amina”
Ikiwa
umeisema sala hii kwa imani, basi sasa wewe umeokoka na dhambi zako
zimesamehewa na kusahauliwa na Mungu sawasawa na alivyoandika katika neno lake.
Jina la Yesu Kristo ni halali yako kulitumia!
Ukipenda unaweza kutuandikia kwa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni